Pages

Wednesday, November 8, 2023

TRA KUANZA KUWASHUKURU WALIPA KODI

Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa kodi na mawasilano TRA, Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa Habari makao makuu ya ofisi zao jijini Dar es Salaam leo Novemba 8, 2023 kuhusu wiki maalum ya kuwashukuru na kuwapongeza walipa kodi kwa hiari na wakati itakayoanza Tar 18 hadi 24 siku ya kilele chake.


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) leo Novemba 08, 20223 imeanza Wiki ya shukrani kwa mlipakodi ambapo itatambua walipakodi wao waliofanya vizuri katika mwaka wa fedha wa 2022/23.

TRA hutumia wiki hiyo kuwatambua wale waliolipa kodi kwa hiari na wale waliotoa ushirikiano wa kutosha kulipa kodi lengo ni kuwatia hamasa walipakodi wote waliolipa kodi zao kwa hiari, bila kusukumwa wala kufuatwa fuatwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo amesema kuwa kilele cha wiki hiyo ni Novemba 24, mwaka huu itakayofanyika Mlimani City, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko.

Sambamba hilo, matukio yatakayotangulia kuelekea kilele ni kuwepo kwa shindano la vilabu vya kodi kwa shule za Sekondari za Dar es Salaam na Pwani ambapo shule 59 zitashiriki.

"Hawa ni wale walipakodi waliotoa ushirikiano kwa maofisa wetu ikiwemo kutoa taarifa za ukaguzi na hata ritani pale walipohitajika. Kimsingi hawa ni wale waliotekeleza sheria ya kodi," amesema Kayombo.

Kayombo amesema lengo ni kuhakikisha wanajenga uhiyari wa kulipa kodi kwa vijana wadogo ili wanapokuwa watu wazima wawe walipakodi wazuri.

Amesema vijana hao wanapaswa kufahamu umuhimu wa kulipa kodi kwani wapo watakaokiwa wafanyabiashara, wakandarasi na wafanyakazi ndani ya TRA.

"Tukio la pili ambalo tutalifanya ni matembezi na mbio za shukrani kwa mlipakodi hivyo vikundi mbalimbali vinakaribishwa," amesisitiza.

Pia ameeleza kuwa siku ya kilele watakuwa na makundi ya kitaifa ikiwemo ya washindi, makundi ya kisekta na makundi ya Wilaya na Mikoa lengo kuzingatia kila kundi la mlipakodi.

Amesema mwaka wa fedha uliopita, makundi mbalimbali yalipata tuzo hizo na mshindi wa jumla alitoka kwenye sekta ya fedha na kwamba walipokea maswali mengi kutoka kwa walipakodi kwanini hawakutajwa kwenye tuzo hizo.

Amefafanua kuwa kwa mwaka huu wanaamini watu wengi wanazidi kuhamasika ili waweze kutambulika kwa kazi nzuri ya kulipa kodi, pia kuwaletea heshima na kuaminika kwa wateja wao.

Ameeleza kuwa kaulimbiu kwa mwaka huu ni Kodi yetu, maendeleo yetu, tuwajibike ikilenga watu walipe kodi, wadai risiti wafanyapo manunuzi na kutoa taarifa ya wanaokwepa kodi.

No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates