Pages

Thursday, May 16, 2024

ASKOFU MKUU WA CANTERBURY AOMBA RADHI KWA NIABA YA UINGEREZA KUFUATIA BIASHARA YA UTUMWA ZANZIBAR


Na Maiko Luoga Zanzibar
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglikana Canterbury Justin Welby kwa niaba ya nchi ya Uingereza amewaomba radhi watu wa Zanzibar, Tanzania na nchi za Afrika zilizotoa watumwa, kufuatia madhira waliyopata wakati wa biashara haramu ya utumwa katika kipindi cha miaka ya 1800 iliyopita.

Askofu Welby aliomba radhi hiyo mei 12, 2024 kwenye adhimisho la Misa ya upatanisho iliyofanyika katika Kanisa Kuu Anglikana Kristo Mkunazini Dayosisi ya Zanzibar na kupokea baraka za Mungu kupitia mikono ya Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa.

“Baba Askofu Mkuu wa Tanzania Maimbo Mndolwa, naomba radhi kwa niaba ya Uingereza kufuatia biashara haramu ya utumwa hapa lilipojengwa Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini, kila siku watu wakifika hapa kumwabudu Mungu hukumbuka mateso waliyopata ndugu zao” Askofu Welby.

Alisema Taifa la Uingereza limetenga Paundi milioni 100 ili kuwanufaisha watu wa nchi za Afrika zilizotoa watumwa huku akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha maisha ya wahanga wa biashara haramu ya Utumwa.

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa, kupitia hotuba aliyoitoa mbele ya Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hussein Alli Mwinyi, waumini na ugeni kutoka mataifa ya nje alieleza hali ya maumivu na matendo mabaya waliyofanyiwa waafrika.

“Hapa ilipo madhbahu ndipo ilipokuwa nguzo ya kuwafunga na kuwapiga watumwa walioonesha upinzani wowote ule. Mtumwa wa aina hiyo alipigwa sana mbele ya wote ili kuwaonesha wengine kwamba hawana uhuru. Pale ndugu zetu walitandikwa mijeredi, walitemewa mate na wengine walibamizwa kwa makofi” alisema Askofu Maimbo.

Aidha alimueleza Askofu Mstaafu Suheil wa Kanisa Anglikana Yerusalem na Askofu Mkuu Mstaafu wa Mashariki ya Kati kuwa wengi wa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakinunua na kuuza watumwa walikuwa Waarabu na Wahindi wachache.

Askofu Mkuu Maimbo Tanzania na Tanga alisisitiza umuhimu wa kutunza historia huku akiibua wazo la kuitambua na kuadhimisha Kitaifa siku ya juni 06 kila mwaka ambayo mkataba wa kukomesha biashara ya utumwa ulitiwa saini na aliyekuwa Sultani wa Zanzibar mwaka 1873.

“Nionavyo mimi hii ndio siku ya uhuru wa Afrika, hii ndio siku tukufu ya kuenziwa. Mheshimiwa Rais, ukiona vema, siku hii ipewe heshima kwa kufanya makongamano ya kitaifa kuhusu ubaya wa biashara hiyo na kukemea machipuko mengine ya biashara ya binadamu”

“Kwa upande wa kanisa Anglikana Tanzania, tunatangaza rasmi kwamba tarehe 06 Juni itaingia katika kalendari yetu nasi tutakuwa hapa kila mwaka ifikapo tarehe hiyo kufanya adhmisho katika Kanisa hili” alisema Askofu Mkuu Maimbo Mndolwa.

Kufuatia wazo hilo la kuitambua siku ya Tarehe 06 juni ya kila mwaka kuwa siku ya kukomesha biashara ya utumwa, Rais wa Zanzibar mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliunga mkono na kuielekeza serikali kushirikiana na Kanisa Anglikana kupanga namna bora ya kuiadhimisha siku hiyo maalumu.

Rais Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza ushirikino kwa Taasisi za Dini ikiwemo Kanisa Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na Tanzania kote ili kuweza kufanya shughuli zake kwa uhuru ikiwemo kutoa huduma bora kwa jamii.

Mhashamu Askofu Mkuu Mstaafu Suheil wa Kanisa Anglikana Yerusalem na Askofu Mkuu Mstaafu wa Mashariki ya Kati alionesha kuumizwa na hali ya mapigano yanayoendelea kati ya nchi ya Palestina na Israel, na kuyaomba Mataifa hayo kufanya maridhiano ili kuepuka vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu.

Akitoa salaam za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mhe, George Simbachawene Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alisema, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa Anglikana Tanzania, katika kuwahudumia watanzania kimwili na kiroho.

“Nami naomba nitumie fursa hii kwa niaba ya Serikali kuwapongeza na kushukuru sana Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi zake zote kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwahudumia watanzania tena bila ubaguzi” alieleza Waziri George Simbachawene.



No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates