Saturday, May 18, 2024
MAHAKAMA YA RUFAA YAFUTA HUKUMU YA MIKOPO CHECHEFU
Thursday, May 16, 2024
ASKOFU MKUU WA CANTERBURY AOMBA RADHI KWA NIABA YA UINGEREZA KUFUATIA BIASHARA YA UTUMWA ZANZIBAR

Monday, May 13, 2024
HOTUBA ILIYOTOLEWA JUMAPILI MEI 12, 2024 KATIKA IBADA YA UPATANISHO KATIKA KANISA KUU LA KRISTO MKUNAZINI ZANZIBAR
Mheshimiwa Dr. Hussein Alli Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Mhashamu Justin, Askofu Mkuu wa Cantebury na Mwenyekiti wa Maaskofu Baraza wa Kianglikana Ulimwenguni
Mhashamu Dr. Albert, Askofu wa Lusaka, Askofu Mkuu wa Afrika Kati na Mwenyekiti wa Baraza la makanisa ya Anglikana Afrika
Mhashamu Dr.Dickson, Makamu wa Askofu Mkuu Kanisa Anglikana Tanzania na Askofu wa Central Tanganyika
Mh. Shekhe Saleh Omary, Mufti wa Zanzibar
Mh. Shekhe Hassan Othman Ngwali, Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Maaskofu, makasisi na mashemasi mliopo
Waheshimiwa Mawaziri
Waumini wetu wote
Kwa wenzetu mliosafiri safari ndefu sana kutoka London, Yerusalem, Lusaka na Nairobi, tunawakaribisha sana Zanzibar. Zanzibar ni patamu, raha, na penye heri. Ukiishi katika ulimwengu huu kisha uwe hujawahi fika Zanzibar, ujue una kasoro.
Tupo katika kisiwa ambacho tangu karne ya saba kimekuwa kitovu cha imani na biashara. Wenzetu Waislamu ndio wa kwanza kabisa kufika hapa na wakaipanda imani yao. Ni kwasababu hii tumemualika Muft wa Zanzibar na kadhi Mkuu maana wao wanawakilisha kundi ambalo lilitupokea na kutupa ushirikiano mkubwa. Mheshimiwa Muft na Mh. Kadhi, Mungu awabariki sana. Tunamshukuru sana Mungu pamoja nanyi kwa jinsi ambavyo mmeendeleza utamaduni uliojengwa na watangulizi wetu miaka mingi iliyopita.
Ndugu zangu maaskofu wakuu na wakuu wa nchi zetu, pamoja na Zanzibar kufahamika sana, na wenzetu wakatoliki kutangulia, historia inatutambulisha kwamba Kanisa Anglikana halikuwahi kuwa na mpango wa kuanzisha huduma Zanzibar pamoja na kwamba maeneo ya Seychelles na Afrika Kusini jirani na Zanzibar tayari kanisa Anglikana lilikuwa limejimarisha huko.
Mmishenari wa kwanza wa kanisa Anglikana kuifikia Zanzibar alikuwa Kasisi Johann Ludwig Krapf aliepita hapa mwaka 1844 akielekea Mombasa alikokuwa ametumwa na chama cha Kianglikana kijulikanacho kwa jina la Church Missionary Society kwenda kuanzisha huduma huko Mombasa.
Tukio lililopelekea Zanzibar kupokea Uanglikana lilianzia na kifo cha Askofu Charles Richard Mackenzie, askofu wa kwanza wa chama cha kiangliaka kijulikanacho kwa jina la Universities Mission to Central Africa (U.M.C.A) ambae mwaka 1862 alipata maralia kali akiwa safarini mto zambezi na akafa na kuzikwa huko. Tukio hilo pamoja na kukwama kwa kazi katika milima ya Shire huko Malawi, lilipelekea UMCA kujiondoa huko kwa nia ya kwenda Natal Afrika Kusini kujipanga upya.
Wakati wanakatiza mkondo wa Mto Zambezi kuingia Bahari ya Hindi, Askofu George Tozer aliemrithi Mackenzie, akiwa na rafiki yake Kasisi Edward Steer, jahazi lao lilivumilishwa na upepo wa Monsoon na kuwaswaga hadi hapa mwaka 1864. Kwa hiyo ujio wao haukuwa wa mpango bali wa Roho Mtakatifu mwenyewe.
Mhashamu Askofu Mkuu Justin, tunajua unaijua historia hii maana imeandikwa vizuri katika vitabu vyetu. Sababu ya kuirudia hapa ndio umuhimu wa siku hii na kwa kweli, tunamshukuru Mungu kwamba wewe binafsi, askofu Mkuu Albert na Suheil mmeweza kufika. Tunasikitika tu kwamba Askofu Mkuu Thabo wa Afrika Kusini ambae kanisa lake ndio lilimtoa Askofu Mackenzie na akawekwa wakfu huko Cape Town hakuweza kuungana nasi leo. Kwa wale msiojua, Askofu Mkuu Thabo asili yake ni Zanzibar hivyo tunasikitika kutokuwa nae leo.
Wahashamu Maaskofu wakuu na Waheshiwa wageni wetu, Askofu Tozer alipofika hapa tunapoabudu leo palikuwa soko kuu la kuuzia ndugu zetu waliochukuliwa utumwani kutoka nchi ambazo leo ni Zambia, Tanganyika, Malawi, Rwanda, Burundi na DRC.
Pale juu ilipo madhbahu ndipo ilipokuwa nguzo ya kuwafunga na kuwapiga watumwa walioonesha upinzani wowote ule. Mtumwa wa aina hiyo alifungwa pale, akapigwa sana mbele ya wote ili kuwaonesha wengine kwamba hawana uhuru. Pale ndugu zetu walitandikwa mijeredi, walitemewa mate na wangine walibamizwa kwa makofi.
Askofu Tozer alipokelewa vizuri sana maana tayari Zanzibar ilikuwa na balozi mdogo wa Uingereza ambae alikuwa na urafiki wa karibu sana na Sultan wa Zanzibar ambae wakati huo tayari amejimilikisha visiwa vyote na kutawala sehemu kubwa ya Tanzania Bara. Askofu Tozer alipokwenda kujitambulisha, Sultan alitaka kujua kwanini wazungu wale wako Zanzibar. Askofu alijibu kwamba amefika Zanzibar kuitangaza dini ya nabii Ibrahimu.
Sultan pia aliwakodisha wamishenari wetu jengo la kuanzia shughuli zao ambalo leo linaitwa Mambomsije na ibada ikaanza hapo tarehe 4 Septemba 1864 waafrika wa kwanza wakiwa zawadi iliyotolewa na Sultan kwa misheni. Mambomsije kwa sasa ni hoteli ya kitalii na chumba kilichokuwa chapel ndio kina bei kubwa zaidi kwa sababu ya historia hii.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na wageni wetu, hii ndio historia inayobeba sababu za uhusiano mwema uliojengeka kati ya Waislamu na Waanglikana na Kanisa na serikali hapa Zanzibar. Uwepo wa viongozi wetu wa kitaifa hapa leo umejengwa katika msingi huu ambao, tunamuomba Mungu asiibuke mtu hata mmoja wa kuutikisa kwa namna yoyote ile.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na wageni wetu, katika msingi huo kanisa Anglikana liliendelea kujiimarisha hapa Zanzibar hata kuyafikia maeneo ya Msumbiji, Malawi, Zambia, na sehemu kubwa ya Tanzania Bara. Kutoka hapa pia chama ca CMS kilituma wamishenari kwenda Uganda na hatimae kuifikia Rwanda na Burundi na DRC. Wamishenari walitumia njia kuu tatu:
Kwanza, walinunua watumwa na kuwabatiza,
Pili pale ambapo hawakuwa na fedha walivamia majahazi yaliyobeba watumwa na kuwateka.
Njia ya mwisho waliyotumia ni kuiiba watumwa na kuwabatiza.
Inaweza pia kutumika kutengeneza kufufua njia walizopita watumwa na kuweka kumbukumbu za bandari walizoingizwa katika majahazi kule Bara. Nauona mradi mkubwa kabisa wa kiimani, kitalii na kibiashara. Ama kwa upande wa kanisa, tunatangaza rasmi kwamba tarehe 6 Juni itaingia katika kalendari yetu nasi tutakuwa hapa kila tarehe hiyo kufanya adhmisho katika kanisa hili. Ngoja tuanze tu kwa uchechefu, mema yatakuja mbele ya safari.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na wageni wetu, kusainiwa kwa mkataba wa kukomesha biashara ya utuma kulileta changamoto kubwa mbili kwa misheni ya kanisa hapa Zanzibar. Kwanza, watumwa waliokuwa njiani kuja hapa na wale waliokuwepo tayari hakukuwa na pakuwapelekeka. Misheni ilichukua hatua za haraka kwa kuchangisha fedha ilikununua maeneo ya kuwatunza. Mashamba makubwa ya Buguruni Malapa na Mtoni Shamba (Dar es salaam), Mbweni, wete na Kiungani (Zanzibar), Kilimatinde (Singida), Berega (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Masasi (Mtwara) na Magila na Misozwe huko Tanga yalinunuliwa na Kanisa la Uingereza. Kwa mara nyingine tunashukuru sana Kanisa la Uingereza kwa kusudi la kuwatunza watumwa waliokombolewa.
Changamoto ya pili ambayo iliikumba misheni hapa Zanzibar ni jinsi ya kuwatunza hawa watumwa waliokombolewa. Kwa kuwa fedha hazikutosha, misheni ilianzisha shughuli za kujitegemea. Shughuli kama vile kilimo, kuchoma chokaa, kupasua mawe, ujenzi na shughuli za ndani zilianza katika vijiji hivi vipya vya kikristo.
Mtumwa aliekuwa mgonjwa hakuwa na maana aliekuwa mzima ndie alihitajika sana. Mateso haya yalijenga utegemezi ambao hata leo bado ungali ukiitafuna nchi yetu. Wako watu leo anapomuona mtu mweupe kutoka Ulaya anafikiri ameona Mungu. Wako watu hata wanaogopa kujiita wamezaliwa na watu waliokuwa watumwa na hata wengine wanataka habari hizi zisisimuliwe kana kwamba hakuna kilichotokea maana kwao utumwa ni udharirishaji mkubwa. Kwa kuwa hakuna popote katika historia Kanisa liliomba radhi kwa wazanzibar na nchi zilizotoa watumwa, nikuombe Mhashamu Askofu Mkuu Justin, wakati wa hotuba yako, useme neno kwa niaba ya nchi yako na kanisa.
Kana kwamba hiyo haitoshi, wakoloni walihakikisha waafrika wote wenye uwezo wanawaua. Walimnyonga mtemi wa Wasambaa kule mazinde, wakamua chifu wa Wachaga kule Moshi, wakawaua Bwana Heri kule Tabora wakati wa Vita vya Pangani, waliwaua wapiganaji wa vita vya ukombozi vya MajiMaji kule songea, wakamsaka Mtemi wa wahehe na kuepelekea kifo chake kule Iringa. Walipoona wamewanyamazisha Waafrika, wakaanza kuchukozana na kugombana wao kwa wao na mwaka 1914 Vita Kuu vya kwanza vya Dunia vikaanza kupiganwa katika nchi yetu. Ndugu zetu walibebwa kwenda kupigana vita ambayo haiwahusu, wengi walikufa kwa vita na maslahi yasiyo yao. Wamishenari wetu wote walisombwa wakapakiwa katika malori na gari moshi wakaenda kufungwa Kiboriani Mpwapwa na hatimae wakapigwa kifungo kibaya gereza la Tabora. Walimu wetu waafrika 55 walitembezwa kwa miguu kutoka Tanga mjini hadi Rufiji kupitia handeni, Kiteto, Kondoa, Dodoma na Morogoro. Wengi walikufa njiani kwa njaa na vipigo, wengine wakafa maji katika mto Rufiji walipokuwa wanajaribu kutoroka hata waliorudi wakabaki 11 tu. Padre Petro Limo akiwa gerezani aliteswa hadi jicho likapofuka na mkono mmoja ukapooza. Padre Cecil Majaliwa nae alifungwa gerezani mwaka mzima bila chakula na maji isipokuwa uji tu. Padre Sehoza anaeleza katika kitabu chake “Mwaka katika Mnyororo”
jinsi alivyonyanyaswa gerezani wakati ule. Baada ya vita hivi kwisha viliibuka vita kuu vya pili ambavyo vilipelekea ndugu zetu kwenda kupigana katika nchi za mbali kama vile Bangladeshi na Pakistani. Wengi walifia huko katika vita isiyowahusu. Tunamshukuru Mungu kwamba wakati wa ziara yake mwaka 2023, Rais wa Ujerumani aliomba radhi kwa watanzania. Kwa kuwa taifa la Uingereza halijawahi kutengeneza jambo hili, kupitia misa hii, nimuombe Mhashamu Askofu Mkuu Justin aseme neno kwa Watanzania nikijua kwamba Ubalozi wa Uingereza nao unasikia na utachukua hatua kama hiyo.
Pamoja na madhira haya, sasa umeibuka utumwa mpya tena, vijana wetu kutoka nchi zile zile wakisakwa kwa ahadi za kazi huko ulaya, uarabuni na hata humu humu nchini. Biashara hiyo haramu ya watu kwa jina jipya Human Trafficking imetengenezwa kimtindo kiasi kwamba ni vigumu kuing’amua kwa haraka. Wanajihusisha na biashara hii wanatumia ombwe lililopo la kutokuwepo ajira kama kigezo. Serikali yetu inajitahidi sana kuwashika wale wanaopitia hapa. Hata hivyo shughuli hiyo imelekea magereza yetu kulemewa mno na wahamiaji haramu. Gharama ya kuwatunza watu hawa ni kubwa mno. Nitumie fursa hii kumuomba Mhashamu skofu Mkuu Justin, kutumia uwakilishi wetu kuishawishi UN ione jinsi ya kuisaidia Tanzania kubeba mzigo huu. Pia tuwatake waumini wetu na wenzetu waislamu, tushirikiane kukomesha biashara hii maana wanaofanya biashara hii wengi ni waumini wetu na wanaleta sadaka.
Lakini pia hapa Zanzibar mara kadhaa tumesikia baadhi ya wenzetu wa imani ya Kiislamu wakitaka kila mtu atiii kutokula mchana wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Jambo hili ni baya kwasababu kwa nchi ambayo haina dini na inaheshimu dini za wengine, utalazimishaje kila mtu afuate dini yako? Ni jambo baya pia maana nchi yetu inategemea sana utalii, tukishaanza kuwabagua watu kwa dini zao, tutajikuta tunawapoteza watu hao. Kanisa linaishukuru sana serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ofisi ya Mufti kwa kukemea jambo hili ambalo likiachiliwa lina madhara makubwa.Ni imani yetu viongozi wetu mtaendelea kulipiga vita jambo hili.
Mhashamu Askofu Mkuu Justin, tupo mahali hapa ambapo pia mtu aliefanya kazi kubwa ya kukiandika Kiswahili kwa herufi za Kiingereza amelala kanisa hili. Huyu sio mwingine bali Askofu Edward Steer aliemrithi George Tozer. Askofu Steer ndie mtu wa kwanza kuandika kamusi ya Kiswahili –kiingereza, wa kwanza kutoa Litujia kwa Kiswahili, wa kwanza kufasiri Injili zote nne kwa Swahili. Ni yeye pia aliejenga kanisa hili na yuko hapa amelala. Naamini ananisikia, ngoja nimwite Edward,
Tunakukumbuka leo kwa kazi yako. Jambo linalotusikitisha Mhashamu Askofu Mkuu ni hili, wakati kanisa lako liliwekeza fedha nyingi hapa kukifanya Kiswahili kiwe hivi kilivyo leo, ila hatuoni kikitumiwa katika makutano makuu ya kanisa badala yake tunasikia Kiingereza, kireno na Kifaransa zaidi kaa kwamba Mungu anazungumza lugha hizo tu.
Tunashukuru kwamba kwa mara ya kwanza mlitupa nafasi kuongoza misa kwa Kiswahili katika mkutano mkuu wa kanisa ulimwenguni ujilikanao kwa jina la Lamberth Conference mwaka 1978 na 2021. Tunashukuru kwamba kwa mara ya kwanza Mkutano wa Maaskofu wakuu tumetoa misa kwa Kiswahili kule Rome mwaka huu. Hata hivyo, Kiswahili kinachotumika humo ni cha wenzetu wakenya na wakonga. Tulisikitika hata katika mkutano wa Kanisa Ulimwenguni mfasili hakukuwa na mtanzania hata mmoja. Pengine ofisi ya ACO haijui kwamba kuna utani huku kwamba Kiswahili kilizaliwa Zanzibar, Kikaendeezwa Tanganyika, Kikajaribiwa kuzungumzwa Kenya, kikauawa Uganda na DRC wakakizika kabisa. Sasa unawatumiaje watu waliozika lugha kufanya tafsiri? Tutumie fursa hii kuiomba ACO ishirikiane na Baraza la Kiswahili Zanzibar na Tanzania kuinua Kiswahili katika ulimwengu wa Kianglikana.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na wageni wetu, ninapoelekea mwisho wa hotuba yetu, hebu sasa tuigeukie Biblia. Katika Biblia kipo kisa cha majibizano ya Yesu Kristo na Masadukayo kuhusu kama ilikuwa halali kumpa Kaisari kodi. Katika kisa hicho Yesu aliwaomba wampe dinari na alipoishika akawageukia akawauliza, sahihi na sanamu iliyokuwa juu ya dinari ilikuwa ya nani na wawakamjibu ni ya kaisari. Yesu akawaambia basi mpeni kaisri iliyo haki yake na Mungu haki yake(Math.22:15-21).
Nichukue fursa hii kuomba tena Mungu atusamehe kwa wizi huo. Bahati mbaya sana, hakuna shughuli yoyote ya kijamii ambayo unaiona hapa ikifaywa kwa kutumia fedha hizo maana ingelikuwepo tungelikuwa na udhuru kwa serikali.
Kwa kuwa tumeiba vyakutosha na kwa kuwa hatuwezi kurudisha tulichoiba, nitumie fursa hii kumuomba Mh. Rais wa Zanzibar kwanza atamke neno la kutusamehe kabisa kabisa na irekodiwe vizuri. Pili tumuombe achukue hatua madhubuti ili serikali ipate haki yake na kanisa lipate haki yake hapa. Tatu tumuombe alihakikishie kanisa kwamba shughuli hiyo ya kupata kodi kutoka hapa haitaathiri shughuli za kanisa wala kuingilia uhuru wa ibada na hiyo nayo irekodiwe vizuri.
Mwisho na sio kwa umuhimu, naleta mamobi yafauatayo kwa serikali yetu na kwa kanisa la Uingereza:
1. Kwa kuwa Juni 6 ndio siku mkataba wa kukomesha biashara ya utumwa ulipotwa saini hapa Unguja na biashara hiyo kuharamishwa kabisa, napendekeza siku hii ipewe hadhi yake. Mheshimiwa Rais, mkiona vema tungeweza kufanya kazi jambo hili na mimi naona fedha itakayokuja hapo baadae sisi tukiwa hatupo. Naiona fedha ndefu hapa kama tukiiundia miundo mbinu. Ziko shughuli ambazo hazijafanywa vyakutosha. Professor Shimvji anasema kweli kwamba eneo la historia ya shughuli za dini na maingliano yake na serikali yakifanyiwa tafiti vizuri, yanaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya serikali na sisi tunaona ukweli huo kwa kuanzia na jambo hili.
3. Kwa kuwa ziko kelele nyingi kuhusu ajira kwa vijana wa Kikristo kutopewa nafsi, tunaishuri serikali ilifanyie kazi jambo hili kuleta usawa na kupunguza kelele.
Saturday, May 11, 2024
ASKOFU MKUU WA KANISA ANGLIKANA JUSTIN WELBY AWASILI ZANZIBAR

*Atembelea maeneo yaliyoendesha biashara ya watumwa.
Na Maiko Luoga Zanzibar.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa mei 10, 2024 aliongoza jopo la Maaskofu na waumini wa Dayosisi ya Zanzibar, kumpokea Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby katika uwanja wa ndege wa kimataifa Zanzibar.
Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby amewasili nchini Tanzania kupitia Dayosisi ya Zanzibar, kwa lengo la kutembelea na kuona maeneo ya kihistoria mahali lilipo Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini Unguja yaliyotumika kufanya biashara haramu ya watumwa.
Mara baada ya kutembea na kupata historia ya maeneo hayo Askofu Mkuu wa Canterbury alisema “Nimetembelea eneo la soko la zamani la watumwa Zanzibar, sasa ni kanisa, ambapo ukatili wa zamani uliofanywa hapa unasikitisha na kumbukwa kikamilifu”.
“Athari ya dhambi ni kubwa zaidi kuliko tunavyoweza kujua. Matokeo ya uovu wa utumwa ni zaidi ya ufahamu. Hii inaweza kusababisha watu kutazama mbali. Hata hivyo, ni lazima tukabiliane na maisha yetu ya zamani kwa uaminifu”.
“Hakika, ni pale tu tunapofanya hivyo, ndipo tunaweza kujua ukombozi kwa maana wokovu daima unahusisha kukiri kwetu, toba, na nia ya kuishi kulingana na Ufalme wa Mungu. Mungu aturehemu ili tutende haki, tupende rehema, na tuenende kwa unyenyekevu pamoja na Mungu wetu” alieleza Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby.
Jumapili mei 12, 2024 katika Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini Zanzibar, itafanyika Misa ikihusisha viongozi wa dini na serikali pamoja na Askofu Mkuu wa Canterbury ili kuomba toba kwa Mungu kufuatia makosa yaliyofanywa na wahusika walioongoza biashara haramu ya watumwa.