HOTUBA ILIYOTOLEWA NA MHASHAMU BABA ASKOFU MAIMBO TANZANIA NA TANGA KATIKA KANISA KUU LA KRISTO MKUNAZINI ZANZIBAR
JUMAPILI
YA KUPAA MEI 12, 2024 IBADA YA UPATANISHO
Mheshimiwa Dr. Samia Hassan
Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Mheshimiwa Dr. Hussein Alli
Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Mhashamu Justin, Askofu Mkuu
wa Cantebury na Mwenyekiti wa Maaskofu Baraza wa Kianglikana Ulimwenguni
Mhashamu Suheil, Askofu
Mstaafu wa Yerusalem na Askofu Mkuu Mstaafu wa Mashariki ya Kati
Mhashamu Dr. Albert, Askofu
wa Lusaka, Askofu Mkuu wa Afrika Kati na Mwenyekiti wa Baraza la makanisa ya
Anglikana Afrika
Mhashamu Dr.Dickson, Makamu
wa Askofu Mkuu Kanisa Anglikana Tanzania na Askofu wa Central Tanganyika
Mh. Shekhe Saleh Omary, Mufti
wa Zanzibar
Mh. Shekhe Hassan Othman
Ngwali, Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Maaskofu, makasisi na mashemasi
mliopo
Waheshimiwa Mawaziri
Waumini wetu wote
Wageni wetu wote
Waandishi wa Habari
Tunawakaribisha katika kanisa
kuu la Kristo hapa Mkunzani
Kwa wenzetu mliosafiri safari
ndefu sana kutoka London, Yerusalem, Lusaka na Nairobi, tunawakaribisha sana
Zanzibar. Zanzibar ni patamu, raha, na penye heri. Ukiishi katika ulimwengu huu
kisha uwe hujawahi fika Zanzibar, ujue una kasoro.
Mhashamu Askofu Mkuu Suheil,
wewe ni mwenyeji wa Palestina, tunajua unakotoka kuna machafuko makubwa na
ndugu zetu wengi kule wamekufa, kwa heshima yao, na wewe mwenyewe, niombe
tusimame kwa sekunde chache.
Tumekusanyika hapa leo ili
kumletea Mungu sala na maombi yetu maana ni kwa huruma na neema zake tu,
aliiumba Zanzibar na kwa wakati aliochagua yeye, akatuma wamishenari kuja
kuujenga ufalme wake hapa.
Tupo katika kisiwa ambacho
tangu karne ya saba kimekuwa kitovu cha imani na biashara. Wenzetu Waislamu
ndio wa kwanza kabisa kufika hapa na wakaipanda imani yao. Ni kwasababu hii
tumemualika Muft wa Zanzibar na kadhi Mkuu maana wao wanawakilisha kundi ambalo
lilitupokea na kutupa ushirikiano mkubwa. Mheshimiwa Muft na Mh. Kadhi, Mungu
awabariki sana. Tunamshukuru sana Mungu pamoja nanyi kwa jinsi ambavyo
mmeendeleza utamaduni uliojengwa na watangulizi wetu miaka mingi iliyopita.
Historia inaonesha kwamba
wamishenari wakikristo wa kwanza kuifikia Zanzibar walikuwa Wakatoliki wakati
wakipita kwenda India mnamo karne ya 16. Ingawa wenzetu hao waliacha alama
katika visiwa hivi na kule Pwani ya Bara, lakini hawakuacha kanisa. Utume wa
Kikatoliki ulioweza kuanzisha kanisa hapa ni ule uliofika mwaka 1860
wakiwatangulia Waanglikana. Kwa heshima ya utangulizi huo, tumemwalika Askofu
wa Jimbo Katoliki Zanzibar ambae pia ni rafiki mwema sana kwa huduma hapa
Zanzibar.
Ndugu zangu maaskofu wakuu na
wakuu wa nchi zetu, pamoja na Zanzibar kufahamika sana, na wenzetu wakatoliki
kutangulia, historia inatutambulisha kwamba Kanisa Anglikana halikuwahi kuwa na
mpango wa kuanzisha huduma Zanzibar pamoja na kwamba maeneo ya Seychelles na
Afrika Kusini jirani na Zanzibar tayari kanisa Anglikana lilikuwa limejimarisha
huko.
Mmishenari wa kwanza wa
kanisa Anglikana kuifikia Zanzibar alikuwa Kasisi Johann Ludwig Krapf aliepita
hapa mwaka 1844 akielekea Mombasa alikokuwa ametumwa na chama cha Kianglikana
kijulikanacho kwa jina la Church Missionary Society kwenda kuanzisha huduma
huko Mombasa.
Tukio lililopelekea Zanzibar
kupokea Uanglikana lilianzia na kifo cha Askofu Charles Richard Mackenzie,
askofu wa kwanza wa chama cha kiangliaka kijulikanacho kwa jina la Universities
Mission to Central Africa (U.M.C.A) ambae mwaka 1862 alipata maralia kali akiwa
safarini mto zambezi na akafa na kuzikwa huko. Tukio hilo pamoja na kukwama kwa
kazi katika milima ya Shire huko Malawi, lilipelekea UMCA kujiondoa huko kwa
nia ya kwenda Natal Afrika Kusini kujipanga upya.
Wakati wanakatiza mkondo wa
Mto Zambezi kuingia Bahari ya Hindi, Askofu George Tozer aliemrithi Mackenzie,
akiwa na rafiki yake Kasisi Edward Steer, jahazi lao lilivumilishwa na upepo wa
Monsoon na kuwaswaga hadi hapa mwaka 1864. Kwa hiyo ujio wao haukuwa wa mpango
bali wa Roho Mtakatifu mwenyewe.
Msafara wa Askofu Tozer
ulipofika hapa ulivutiwa na hivyo wakaamua kubaki uamuzi ambao haukukubaliwa
hata kidogo na waliomtuma wakimshutumu kwamba ana nia ya kukwamisha mpango wa
Mungu na kanisa. David Livingstone ambae nia yake ya kubadili kukomesha
biashara ya utumwa na kuwastaarabisha waafrika wanaouzana wao kwa wao na ambae hotuba
yake ndio iliyopelekea UMCA kuundwa alimshutumu vikali Tozer. Hata hivyo, Tozer alisimamia maamuzi yake
wakabaki hapa.
Mhashamu Askofu Mkuu Justin,
tunajua unaijua historia hii maana imeandikwa vizuri katika vitabu vyetu.
Sababu ya kuirudia hapa ndio umuhimu wa siku hii na kwa kweli, tunamshukuru
Mungu kwamba wewe binafsi, askofu Mkuu Albert na Suheil mmeweza kufika.
Tunasikitika tu kwamba Askofu Mkuu Thabo wa
Afrika Kusini ambae kanisa lake ndio lilimtoa Askofu Mackenzie na
akawekwa wakfu huko Cape Town hakuweza
kuungana nasi leo. Kwa wale msiojua, Askofu Mkuu Thabo asili yake ni Zanzibar
hivyo tunasikitika kutokuwa nae leo.
Wahashamu Maaskofu wakuu na
Waheshiwa wageni wetu, Askofu Tozer alipofika hapa tunapoabudu leo palikuwa
soko kuu la kuuzia ndugu zetu waliochukuliwa utumwani kutoka nchi ambazo leo ni
Zambia, Tanganyika, Malawi, Rwanda, Burundi na DRC.
Pale juu ilipo madhbahu ndipo
ilipokuwa nguzo ya kuwafunga na kuwapiga watumwa walioonesha upinzani wowote
ule. Mtumwa wa aina hiyo alifungwa pale,
akapigwa sana mbele ya wote ili kuwaonesha wengine kwamba hawana uhuru. Pale
ndugu zetu walitandikwa mijeredi, walitemewa mate na wangine walibamizwa kwa
makofi.
Askofu Tozer alipokelewa
vizuri sana maana tayari Zanzibar ilikuwa na balozi mdogo wa Uingereza ambae
alikuwa na urafiki wa karibu sana na Sultan wa Zanzibar ambae wakati huo tayari
amejimilikisha visiwa vyote na kutawala sehemu kubwa ya Tanzania Bara. Askofu Tozer alipokwenda kujitambulisha,
Sultan alitaka kujua kwanini wazungu wale wako Zanzibar. Askofu alijibu kwamba
amefika Zanzibar kuitangaza dini ya nabii Ibrahimu.
Sultan
ambae nae alikuwa mfuasi wa dini ya Kiislamu ambayo ina mizizi yake katika dini
hiyo ya Ibrahimu, alifurahi na kwa hiyo akampatia zawadi ya watumwa vijana
watano (Swedi, Feruzi, Farijallah, Songoro and Mabruki).
Sultan pia aliwakodisha
wamishenari wetu jengo la kuanzia shughuli zao ambalo leo linaitwa Mambomsije
na ibada ikaanza hapo tarehe 4 Septemba 1864 waafrika wa kwanza wakiwa zawadi
iliyotolewa na Sultan kwa misheni. Mambomsije kwa sasa ni hoteli ya kitalii na
chumba kilichokuwa chapel ndio kina bei kubwa zaidi kwa sababu ya historia hii.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na
wageni wetu, hii ndio historia inayobeba sababu za uhusiano mwema uliojengeka
kati ya Waislamu na Waanglikana na Kanisa na serikali hapa Zanzibar. Uwepo wa
viongozi wetu wa kitaifa hapa leo umejengwa katika msingi huu ambao, tunamuomba
Mungu asiibuke mtu hata mmoja wa kuutikisa kwa namna yoyote ile.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na
wageni wetu, katika msingi huo kanisa Anglikana liliendelea kujiimarisha hapa
Zanzibar hata kuyafikia maeneo ya Msumbiji, Malawi, Zambia, na sehemu kubwa ya
Tanzania Bara. Kutoka hapa pia chama ca CMS kilituma wamishenari kwenda Uganda
na hatimae kuifikia Rwanda na Burundi na DRC. Wamishenari walitumia njia kuu
tatu:
Kwanza, walinunua watumwa na
kuwabatiza,
Pili pale ambapo hawakuwa na
fedha walivamia majahazi yaliyobeba watumwa na kuwateka.
Njia ya mwisho waliyotumia ni
kuiiba watumwa na kuwabatiza.
Njia hizi zilitumika kwa
miaka minane hadi mwaka 1873 Biashara ya Utumwa ilipoharamishwa na kupigwa
marufuku huko Westminster Abby. Tarehe 6 Juni mwaka 1873, Sultan wa Zanzibar
akatia saini mkataba na kuharamisha rasmi Biashara ya Utumwa katika milki yake.
Miezi mitatu baadae tarehe 5 Septemba mwaka 1873, Kasisi A. N. West mmoja wa
familia tajiri za Buckingham huko Uingereza, alinunua sehemu ya soko hili
iliyokuwa na nguzo ya kutesea watumwa na eneo lilo wazi na kuikabidhi kwa
misheni.
Familia ya ya Kihindu ya Jairam Senji, mmoja wa wafanyabiashara tajiri
Zanzibar wakati huo na ambayo ilikuwa ikimiliki nyumba moja kubwa hapa na eneo
la wazi la kutunzia watumwa, ilitoa nyumba hiyo na sehemu hiyo kuwa zawadi kwa
misheni. Kanisa Anglikana Tanzania, linaishukuru sana familia ya Senji na West
kwa heshima waliyoipa Kanisa la Zanzibar. Leo tumemualika mmoja wa wanafamilia
wa Senji ili kuishukuru familia hii kwa mara nyingine.
Lakini pia shukrani zetu
uzipokee wewe Mhashamu Askofu Mkuu Justin kwa jinsi ambavyo kanisa lako
lilikusanya fedha kwa haraka sana na kuweka jengo hapa la kipekee kabisa kwa
ukanda huu wa Afrika. Jengo hili la mtindo wa Basilika iliyotengenezwa kwa
kuchanganya utamaduni wa kigothiki na kiarabu ni urithi wa kipekee sana. Kama
tulivyoeleza mwanzoni kwamba hata ile madhbahu pale ilipo imebeba heshima ya
kipekee sana na ujumbe ambao huukuti popote katika kanisa hapa duniani. Ni pale
pale walippopigwa ndugu zetu, ndipo Kristo ajitoapo kwa ajili yetu akitujia
katika fumbo la mkate na divai.
Ni palepale ambapo damu za ndugu zetu
zilimwagika, ndipo tubarikipo divai kuwa damu ya Yesu Kristo, ni palepale
walipouzwa wasiokosa, ndipo ajitoapo mwanakondoo wa Mungu ili auponye
ulimwengu. Natamani theolojia hii ambayo
hatuna kanisa jingine popote duniani isambae kotekote iwalete mahujaji hapa,
wajue jinsi Zanzibar ilivyo kuu na utukufu. Katika ubeti wa 4 wa Nyimbo za Dini
499 mwandishi anakamata wazo hili:
Twapenda meza ile
Tukuonapo, Bwana
Hapana kama hapa
Popote duniani
Ubeti wa sita wa wimbo huo
huo nao ubeba shangwe ile ile:
Twapenda
kuziimba
Rehema tupewazo
Twataka kuzijua
Wanazoimba juu
Ndio maana sisi wengine
tunapata taabu sana kusikia wako wanaochezea mahali hapa na kupafanya kama ni
mahali pa mchezo mchezo tu. Kama kuna mahali posipopaswa kuchezewa ni mahali
hapa. Kwasababu ya upekee wa mahali hapa na ile tarehe 6 juni, tunaleta ombi
kwa kanisa na serikali. Tarehe 6 Juni ndio siku ambayo Mkataba wa Kukomesha
biashara ya utumwa ulitiwa saini hapa Zanzibar.
Nionavyo mimi hii ndio siku ya
uhuru wa Afrika. Nionavyo mimi hii ndio siku tukufu kabisa ya kuenziwa.
Mheshimiwa Rais, ukiona vema, siku hii ipewe heshima kwa kufanya makongamano ya
kitaifa kuhusu ubaya wa baiashara hiyo na kukemea machipuko mengine ya biashara
ya binadamu.
Inaweza pia kutumika
kutengeneza kufufua njia walizopita watumwa na kuweka kumbukumbu za bandari
walizoingizwa katika majahazi kule Bara. Nauona mradi mkubwa kabisa wa kiimani,
kitalii na kibiashara. Ama kwa upande wa kanisa, tunatangaza rasmi kwamba tarehe
6 Juni itaingia katika kalendari yetu nasi tutakuwa hapa kila tarehe hiyo
kufanya adhmisho katika kanisa hili. Ngoja tuanze tu kwa uchechefu, mema
yatakuja mbele ya safari.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na
wageni wetu, kusainiwa kwa mkataba wa kukomesha biashara ya utuma kulileta
changamoto kubwa mbili kwa misheni ya kanisa hapa Zanzibar. Kwanza, watumwa
waliokuwa njiani kuja hapa na wale waliokuwepo tayari hakukuwa na
pakuwapelekeka. Misheni ilichukua hatua za haraka kwa kuchangisha fedha
ilikununua maeneo ya kuwatunza. Mashamba makubwa ya Buguruni Malapa na Mtoni
Shamba (Dar es salaam), Mbweni, wete na Kiungani (Zanzibar), Kilimatinde
(Singida), Berega (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Masasi (Mtwara) na Magila na
Misozwe huko Tanga yalinunuliwa na Kanisa la Uingereza. Kwa mara nyingine
tunashukuru sana Kanisa la Uingereza kwa kusudi la kuwatunza watumwa
waliokombolewa.
Changamoto ya pili ambayo
iliikumba misheni hapa Zanzibar ni jinsi ya kuwatunza hawa watumwa
waliokombolewa. Kwa kuwa fedha hazikutosha, misheni ilianzisha shughuli za
kujitegemea. Shughuli kama vile kilimo, kuchoma chokaa, kupasua mawe, ujenzi na
shughuli za ndani zilianza katika vijiji hivi vipya vya kikristo.
Hata hivyo,
kwa kuwa wana vijiji hawa waliishi maisha ya utumwa hapo kwanza, wakajikuta wamisheni
wanawatumikisha watu hawa kama watumwa tu. Waliamshwa kabla jua kuchomoza kwa
ajili ya sala na misa, kisha ikafuata usafi na kisha kazi na kufuatiwa na sala
nyingi na kazi. Hapa ndipo ilizaliwa
falsafa ya kazi na sala.
Mateso yalikuwa makubwa maana kila aliekosa kusali
aliadhibiwa sawa na ambae hakufanya kazi yake sawasawa. Waliopinga jambo hili
walifukuzwa na mmoja wa waliofukuzwa ni miongoni mwa wale vijana watano wa
kwanza aliopokea Askofu Tozer. Zaidi ya hayo, kwa kuwa UMCA ilizuia wamishenari
kuoa au kuolewa, baadhi ya wamishenari wasiojiheshimu walifanya zinaa na wana
vijiji hawa wapya na ilipogundulika wamishenari walifukuzwa ila hawa watoto na
wazazi wao wakawa mali ya misheni.
Wamishenari wakajipatia
heshima hata kuwaita watu hawa waliokuwa wakiwatumikia kuwa ni wa kwao. Maneno
kama vile my boy, my girl, tone boy yanayoonesha umiliki wa watu hao wakati
ule. Hali ilivyokuwa katika vijiji vya
Kikristo ndio pia iliyokuwa kwa watumwa waliokuwa wanafanyakazi katika mashambani
na nyumba za wenzetu waarabu na wahindi.
Mtumwa aliekuwa mgonjwa
hakuwa na maana aliekuwa mzima ndie alihitajika sana. Mateso haya yalijenga
utegemezi ambao hata leo bado ungali ukiitafuna nchi yetu. Wako watu leo
anapomuona mtu mweupe kutoka Ulaya anafikiri ameona Mungu. Wako watu hata
wanaogopa kujiita wamezaliwa na watu waliokuwa watumwa na hata wengine wanataka
habari hizi zisisimuliwe kana kwamba hakuna kilichotokea maana kwao utumwa ni
udharirishaji mkubwa. Kwa kuwa hakuna popote katika historia Kanisa liliomba
radhi kwa wazanzibar na nchi zilizotoa watumwa, nikuombe Mhashamu Askofu Mkuu
Justin, wakati wa hotuba yako, useme neno kwa niaba ya nchi yako na kanisa.
Mhashamu Askofu Mkuu Mstaafu
Suheil, wakati Askofu Tozer anafika hapa, wengi wa wafanyabiashara wakubwa waaliokuwa
wakiuza na kununua watumwa walikuwa Waarabu na Wahindi wachache. Chini yao
walikuwa makundi ya waasia wengi na Wafrika.
Kama tulivyoeleza mwanzo, watumwa waliuzwa hapa. Njia pekee ya kuepuka kuuzwa
ilikuwa ni kuwa Muislamu maana usilamu unakataza kuuza muislamu utumwani. Kwa
bahati mbaya sana, waanzilishi wa biashara hii walitumia biblia
kuiharalisha. Biashara hapa ilianza saa
kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.
Majahazi yaliyobeba watumwa
yaliyofika jioni sana yalishusha watumwa na wakafungiwa katika mapango kumi na
mawili yaliyokuwa katika jengo letu hapo nje (tumebakisha mapango mawili baada
ya kufukia mengine yote wakati wa ujenzi. Hali ilivyokuwa katika mapango
inasikitisha: Padre Steer anaeleza jinsi hali ilivyokuwa: “niliona watumwa kwa
maelefu wamelala chini wamechoka sana, wengine wana vidonda miguuni na wengine
majeraha midomoni, pengine kwa kupigwa huko njiani.
Wengi wao wamefungwa
minyororo na magongo shingoni ili wasitoroke. Inasikitisha sana kuoa hali hii.
Asubuhi waliletwa kuuzwa kwa mnada na wakasafirishwa kwenda Uarabuni baada ya
kulipiwa ushuru kama bidhaa vile.” Walipofika huko wanaume walihasiwa ili
wasije wakazaa na wake za mabwana wao. Wanawake wengi waligeuzwa kuwa watumwa
king’ono. Waliopata mimba kwa bahati mbaya waliuawa kwa kificho. Kisa kimoja
kilichoandikwa kinaonesha mwanamke mjamzito alieuwa na kupasuliwa ili watoto wa
bwana wake waone jinsi mtoto anavyoishi tumboni. Matendo haya mabaya yasiyo ya
utu, yametendwa kwa ndugu zetu. Waliotenda hawapo tena, ila sisi tupo hivyo ni
kuombe Mhashamu Suheil wakati ukisimama useme neno la msamaha kwa makosa haya
ya kibinadamu.
Wahashamu maaskofu wakuu na
wageni wetu, tunapomshukuru Mungu kwa kuisha biashara ile ya utumwa, tusisahau
kwamba waliotutawala walibaili mbinu tu. Tusisahahu Mkutano wa Berlin ulioigawa
Afrika kwa mataifa ya ulaya ulivyoleta changamoto nyingine. Historia
inatuonesha kwamba ukoloni ulibeba dhana ya ubepari, ubeberu na ukandamizaji na
hivyo yakaanzishwa mashamba makubwa ya Kahawa, Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku,
Katani, Karanga na Mpira kwa ajili ya kuzalisha mali ghafi kwa viwanda vyao huko
ulaya. Watu wa kuhudumia mashamba haya hawakuwepo hivyo ilibidi kuwatafuta.
Utumwa mpya ulianza hapa. Watu waliletwa kwa gari la moshi na malori kutoka
Malawi, Rwanda, Burundi, DRC na Zambia (nchi zile zile tena zilizotoa watumwa
hapo kwanza). Ili kuweka kumbukumbu za nchi walizotoka na mashambani waliko,
walipewa namba na jina manamba likanzia hapa. Wenye mashamba walijenga kambi na
kuwaweka huko ili wafanye kazi kwa ufanisi. Kwa kuwa wengi walikuwa wanaume,
wengi walitoroka usiku na kuvamia wake za watu katika vijiji vya kikristo,
kiislamu na kimila na kuzalisha ugomvi mkubwa. Serikali ya kikoloni iliingilia
kati kwa kuleta wanawake kutoka nchi hizo hizo na kuwaweka katika kambi
hizo na kizazi kipya kikaanza. Baada ya
uhuru na utaifishaji mashamba haya, watu hawa hawakuweza kurudi walikotoka na
matokeo yake wamo katika makambi hayo na kuanzisha uzao ambao kwa kweli hauna
identity.
Kana kwamba hiyo haitoshi, wakoloni
walihakikisha waafrika wote wenye uwezo
wanawaua. Walimnyonga mtemi wa Wasambaa kule mazinde, wakamua chifu wa
Wachaga kule Moshi, wakawaua Bwana Heri kule Tabora wakati wa Vita vya Pangani,
waliwaua wapiganaji wa vita vya ukombozi vya MajiMaji kule songea, wakamsaka
Mtemi wa wahehe na kuepelekea kifo chake kule Iringa. Walipoona
wamewanyamazisha Waafrika, wakaanza kuchukozana na kugombana wao kwa wao na
mwaka 1914 Vita Kuu vya kwanza vya Dunia vikaanza kupiganwa katika nchi yetu.
Ndugu zetu walibebwa kwenda kupigana vita ambayo haiwahusu, wengi walikufa kwa
vita na maslahi yasiyo yao. Wamishenari wetu wote walisombwa wakapakiwa katika
malori na gari moshi wakaenda kufungwa Kiboriani Mpwapwa na hatimae wakapigwa
kifungo kibaya gereza la Tabora. Walimu wetu waafrika 55 walitembezwa kwa miguu
kutoka Tanga mjini hadi Rufiji kupitia handeni, Kiteto, Kondoa, Dodoma na
Morogoro. Wengi walikufa njiani kwa njaa na vipigo, wengine wakafa maji katika
mto Rufiji walipokuwa wanajaribu kutoroka hata waliorudi wakabaki 11 tu. Padre
Petro Limo akiwa gerezani aliteswa hadi jicho likapofuka na mkono mmoja
ukapooza. Padre Cecil Majaliwa nae alifungwa gerezani mwaka mzima bila chakula
na maji isipokuwa uji tu. Padre Sehoza anaeleza katika kitabu chake “Mwaka
katika Mnyororo”
jinsi alivyonyanyaswa
gerezani wakati ule. Baada ya vita hivi kwisha viliibuka vita kuu vya pili
ambavyo vilipelekea ndugu zetu kwenda kupigana katika nchi za mbali kama vile
Bangladeshi na Pakistani. Wengi walifia huko katika vita isiyowahusu. Tunamshukuru
Mungu kwamba wakati wa ziara yake mwaka 2023, Rais wa Ujerumani aliomba radhi kwa
watanzania. Kwa kuwa taifa la Uingereza halijawahi kutengeneza jambo hili,
kupitia misa hii, nimuombe Mhashamu Askofu Mkuu Justin aseme neno kwa
Watanzania nikijua kwamba Ubalozi wa Uingereza nao unasikia na utachukua hatua
kama hiyo.
Pamoja na madhira haya, sasa
umeibuka utumwa mpya tena, vijana wetu kutoka nchi zile zile wakisakwa kwa
ahadi za kazi huko ulaya, uarabuni na hata humu humu nchini. Biashara hiyo
haramu ya watu kwa jina jipya Human
Trafficking imetengenezwa kimtindo kiasi kwamba ni vigumu kuing’amua kwa
haraka. Wanajihusisha na biashara hii
wanatumia ombwe lililopo la kutokuwepo ajira kama kigezo. Serikali yetu
inajitahidi sana kuwashika wale wanaopitia hapa. Hata hivyo shughuli hiyo
imelekea magereza yetu kulemewa mno na wahamiaji haramu. Gharama ya kuwatunza
watu hawa ni kubwa mno. Nitumie fursa hii kumuomba Mhashamu skofu Mkuu Justin,
kutumia uwakilishi wetu kuishawishi UN ione jinsi ya kuisaidia Tanzania kubeba
mzigo huu. Pia tuwatake waumini wetu na wenzetu waislamu, tushirikiane
kukomesha biashara hii maana wanaofanya biashara hii wengi ni waumini wetu na
wanaleta sadaka.
Wahashamu Maaskofu Wakuu na
wageni wetu, Utumwa mwingine mbaya unaibuka ni ubaguzi wa kidini. Pamoja na
serikali yetu kutokuwa na dini, watu wake wanaamini dini. Watu kuwa na dini zao
inasaidia serikali kuwa na watu waaminifu. Kazi kubwa ya kila dini ni kuwavuta
wasio wa dini hiyo waingie. Kinachosikitisha ni matumizi ya nguvu kuwafanya
watu watii dini fulani. Hivi karibuni kuliibuka kundi la wafausi wa dini ya
asili huko Kigoma wakijiita lambalamba ambao wamekuwa wakiwalazimisha watu
wafuate amri zao. Waliowapinga walizushia kwamba ni wachawi hivyo waliwapiga na
kuwadharirisha hadharani. Kanisa limeinua sauti na kuandika kukemea jambo hili
lakini hatuja sikia kiongozi yeyote wa serikali akilisemea jambo hili.
Lakini pia hapa Zanzibar mara kadhaa tumesikia
baadhi ya wenzetu wa imani ya Kiislamu wakitaka kila mtu atiii kutokula mchana
wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Jambo hili ni baya kwasababu kwa nchi ambayo haina dini na inaheshimu
dini za wengine, utalazimishaje kila mtu afuate dini yako? Ni jambo baya pia
maana nchi yetu inategemea sana utalii, tukishaanza kuwabagua watu kwa dini
zao, tutajikuta tunawapoteza watu hao. Kanisa linaishukuru sana serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Ofisi ya Mufti kwa kukemea jambo hili ambalo likiachiliwa
lina madhara makubwa.Ni imani yetu viongozi wetu mtaendelea kulipiga vita jambo
hili.
Mhashamu Askofu Mkuu Justin,
tupo mahali hapa ambapo pia mtu aliefanya kazi kubwa ya kukiandika Kiswahili
kwa herufi za Kiingereza amelala kanisa hili. Huyu sio mwingine bali Askofu
Edward Steer aliemrithi George Tozer. Askofu Steer ndie mtu wa kwanza kuandika
kamusi ya Kiswahili –kiingereza, wa kwanza kutoa Litujia kwa Kiswahili, wa
kwanza kufasiri Injili zote nne kwa Swahili. Ni yeye pia aliejenga kanisa hili
na yuko hapa amelala. Naamini ananisikia, ngoja nimwite Edward,
Tunakukumbuka leo kwa kazi
yako. Jambo linalotusikitisha Mhashamu Askofu Mkuu ni hili, wakati kanisa lako
liliwekeza fedha nyingi hapa kukifanya Kiswahili kiwe hivi kilivyo leo, ila
hatuoni kikitumiwa katika makutano makuu ya kanisa badala yake tunasikia
Kiingereza, kireno na Kifaransa zaidi kaa kwamba Mungu anazungumza lugha hizo
tu.
Tunashukuru kwamba kwa mara
ya kwanza mlitupa nafasi kuongoza misa kwa Kiswahili katika mkutano mkuu wa
kanisa ulimwenguni ujilikanao kwa jina la Lamberth Conference mwaka 1978 na 2021. Tunashukuru kwamba kwa
mara ya kwanza Mkutano wa Maaskofu wakuu tumetoa misa kwa Kiswahili kule Rome
mwaka huu. Hata hivyo, Kiswahili kinachotumika humo ni cha wenzetu wakenya na
wakonga. Tulisikitika hata katika mkutano wa Kanisa Ulimwenguni mfasili hakukuwa
na mtanzania hata mmoja. Pengine ofisi ya ACO haijui kwamba kuna utani huku
kwamba Kiswahili kilizaliwa Zanzibar, Kikaendeezwa Tanganyika, Kikajaribiwa
kuzungumzwa Kenya, kikauawa Uganda na DRC wakakizika kabisa. Sasa unawatumiaje
watu waliozika lugha kufanya tafsiri? Tutumie fursa hii kuiomba ACO ishirikiane
na Baraza la Kiswahili Zanzibar na Tanzania kuinua Kiswahili katika ulimwengu
wa Kianglikana.
Mhashamu Askofu Mkuu Justin,
kanisa lako lilituma watu wema wengi. Tunajua wako wachache waliokuwa wahuni na
hao wapo tu siku zote hadi Mwenye kanisa atakaporudi. MMoja wa watu hao ni
Askofu Frank Weston ambae kazi yake hapa Tanzania imemfanya aitwe Mtakatifu. Huduma
ya Askofu Frank ilijaa maajabu na moja ya muujiza aliofanya ni chanzo cha
mapato ya serikali katika Misitu ya Nilo mahali ambapo aligonga mwamba ukatoa
maji wakati wa kiangazi kikali na hayajakauaka hadi leo. Askofu Frank alikuwa
mchungaji mwema kwa watu wake. Siku zote aliwatembelea watu na kusema nao. Ni
yeye pia alianzisha ibada hizi za kuimba. Wakati anaanza kazi hiyo ya
matengenezo ya ibada, kasisi Cecil Majaliwa, babu yake na aliekuwa Askofu wetu
Mkuu John Ramadhani, alichochea wazee wa kanisa hapa wamgomee askofu na hata bidii
yake ya kuanzisha chama cha skauti hapa mwaka 1912 ikakwamishwa na wazee hao.
Matokeo ya mapambano hayo yalipelekea Cecil Majaliwa kutopewa kiti cha Uaskofu
wa Masasi alikuwa ameandaliwa. Hali ya hewa ilipochafuka sana Zanzibar, Frank
aliamua kuondoa kiti cha Uaskofu wa Zanzibar na Makao makuu ya dayosisi
akahamishia Magila huko Mueza Tanga. Wakati anaondoka hapa mwaka 1917, aligonga
fimbo katika madhabahu hii akisema maneno makali kwa Padre Cecil jambo
lililopelekea Padre huyo kuishia vibaya hadi kifo chake na hata familia yake kuathirika.
Frank aliitembelea Zanzibar mara tatu tangu hiyo 1917 hadi alifariki mwaka 1924
na kuzikwa katika kanisa la Magila Msalabani. Mwaka huu tutaadhimisha kazi zake
mwezi Novemba kule Magila.
Frank Weston alirithiwa na
Askofu Thomas Birlye aambae nae alijikuta katika moto aliopitia mtangulizi wake
na kwa hiyo akagoma kuitisha sinodi tangu alipoingia mwaka 1925 hadi amemliza
mwaka 1942 alifanya mkutano mmoja. Thomasi Birley aliisusa Zanzibar kabisa na
akaishi Magila miaka yake yote. Uamuzi wake huo ndio uliopelekea majengo ya
kiungani kuanguka. Mwandishi wa wimbo 505 anagusa kidogo vita alivyopitia
Askofu Thomasi Birley.
Watu waliokaribu na mbali
Watu wajinga
na wenye elimu,
Wanadamu wa kila taifa
Ndie
mwenyezi anaewatunza
Watu
maskini na watu wakubwa
Watu weusi na watu
weupe
Wana
wafalme na wana watumwa
Watu
wamoja machoni pa Mungu
Askofu Birley alishutumiwa
kuwa ana uzungu mwingi na kujidai kwamba ana elimu nyingi na ndio maana
mwandishi wa wimbo huu Rev. Can. Samwil Sehoza, mmoja wa waliopambana na askofu
Birley anataja mambo hayo. Thomas Birley alikataa kutumia fimbo ya Zanzibar
hivyo akajitengenezea ya kwake na alipondoka aliondoka nayo. Aliemrithi Thomas Birley ni William Scott
Backer ambae aliingia katika chenye changamoto nyingi pengine kuliko yeyote
katika waliomtangulia (Movement for Independence, struggle fofr the Independence,
Revolution, Africanization movement, Nationalization).
Askofu William
alijitahidi sana kuirudishia Zanzibar heshima yake lakini haikuwa rahisi.
Kwanza, aliona ilikuwa muhimu kumleta Askofu Msaidizi kuiandaa Zanzibar irudie
heshima yake na kwa hiyo akamwekea mikono Kasisi Neil Russell kuwa askofu mwaka
1963 na kumtuma hapa. Kama alivyokuwa Frank, Russell nae alikuwa mchungaji
mwema sana. Siku zote aliwatembelea Rais Karume na waumini nyumba kwa nyumba
kujua taabu zao. Katika wajibu wake huo, aligundua kwamba waumini wake wanaume
waliokuwa wanafanya kazi serikalini walikuwa na nyumba ndogo na hawakuwa
wanajali matunzo ya familia zao.
Askofu Russell akawaita mmoja mmoja na kuwaonya
jambo ambalo wazee hao na nyumba ndogo hawakutaka na hivyo wakaweka kichungo na
kumshitaki askofu kwa Rais kwamba anapinga Mapinduzi na Africanisation. Askofu
ambae alitoa kanisa hili kuendesha vikao vya siri kuelekea mapinduzi, na ambae
alimsindikiza John Okelo na Sultan hadi Dar es Salaam ili kuinusuru Zanzibar
mara baada ya mapinduzi, akaamriwa aondoke ndani ya masaa 24 mwaka 1964. Askofu
aliondoka hadi bandarini na pale alikimbizwa na walinzi waliokuwa wamepewa amri
na serikali na hapo akaacha viatu vyake. Neil Russell ambae ndie amefungua makanisa
kideleko, Mombo, Mazinde, Kihurio, Mnazi, Mwala na Vunta huko Bara siku zote
ametembea miguu peku na alipoulizwa sababu za kufanya hivyo alisema viatu vyake
walimnyang’anya wazanzibar.
Baada ya
Russell kundolewa Zanzibar kwa fitina za wazee Askofu William aliamua
kuiunganisha Zanzibar na Dsm na hivyo ikaanzishwa Dayosisi ya Zanzibar na Dsm
mwaka 1964 lakini nayo haikudumu maana ilivunjika mwaka uliofuata tu kwa hiyo
Zanzibar ikapelekwa Tanga ikajulikana kuwa Daysosisi ya Zanzibar na Tanga tangu
mwaka 1965 chini ya William. Yohana Jumaa aliemrithi William tangu 1968,
hakuthubutu kurejesha kiti cha Zanzibar hadi alipoingia John Ramadhani ambae
nae jitihada zake tangu mwaka 1980 hazikufanikiwa hadi mwaka 2000 ndipo
akafanikiwa na kuirudishia Zanzibar kiti chake ila fimbo ilibaki Dsm.
Askofu
John alifanikiwa kuiongoza Zanzibar pengine kwa kuwa anatoka katika ukoo
mkubwa. Yeye alirithiwa na Douglas Toto ambae nae alipitia shida nyingi hadi mauti
ya ghafla ilipomkumba. Baadhi yenu mtakumbuka maneno yake katika Kanisa la Mt.
bartholomayo Ubungo Dsm siku chache kabla ya kifo chake. Baada ya kifo cha Douglas Dayosisi ilikosa
askofu kwa miaka 8 ndipo akachaguliwa Michael ambae nae hajamaliza vizuri.
Nimetumia muda mrefu kueleza hapa kwasababu naona yako mambo hayako sawa katika
kiti cha uaskofu wa Zanzibar. Nitumie fursa hii kuomba radhi kwa Askofu Frank,
Masista wa CSP, Askofu Thomas Birley, Askofu William Scott Backer, Neil
Russell, Askofu Douglas Askofu Michael na makasisi Thomas Godda, John Mwamazi
na Noel Ndahani kwa yote waliyopitia hapa. “Ee
Mungu usikiaye kuomba, wewe ambae wote wenye mwili watakujia, usiyakumbuke
makosa yetu, wala makosa ya baba zetu, wala usitupatilize kwa dhambi za watu wako,
utuachilie Bwana mwema, utuachilie sisi watu wako uliotukomboa kwa damu yako ya
thamani na kwa hiyo usituonee ghadhabu.Ni wewe tu Bwana wa kukifungua kiti cha
uaskofu wa Zanzibar, fungua ili kanisa lako lipone. Amin.
Nichukue fursa hii kuomba
tena Mungu atusamehe kwa wizi huo. Bahati mbaya sana, hakuna shughuli yoyote ya
kijamii ambayo unaiona hapa ikifaywa kwa kutumia fedha hizo maana ingelikuwepo
tungelikuwa na udhuru kwa serikali.
Kwa kuwa tumeiba vyakutosha
na kwa kuwa hatuwezi kurudisha tulichoiba, nitumie fursa hii kumuomba Mh. Rais
wa Zanzibar kwanza atamke neno la kutusamehe kabisa kabisa na irekodiwe vizuri.
Pili tumuombe achukue hatua madhubuti ili serikali ipate haki yake na kanisa
lipate haki yake hapa. Tatu tumuombe alihakikishie kanisa kwamba shughuli hiyo
ya kupata kodi kutoka hapa haitaathiri shughuli za kanisa wala kuingilia uhuru
wa ibada na hiyo nayo irekodiwe vizuri.
Mwisho na sio kwa umuhimu,
naleta mamobi yafauatayo kwa serikali yetu na kwa kanisa la Uingereza:
1. Kwa
kuwa Juni 6 ndio siku mkataba wa kukomesha biashara ya utumwa ulipotwa saini
hapa Unguja na biashara hiyo kuharamishwa kabisa, napendekeza siku hii ipewe
hadhi yake. Mheshimiwa Rais, mkiona vema tungeweza kufanya kazi jambo hili na
mimi naona fedha itakayokuja hapo baadae sisi tukiwa hatupo. Naiona fedha ndefu
hapa kama tukiiundia miundo mbinu. Ziko shughuli ambazo hazijafanywa
vyakutosha. Professor Shimvji anasema kweli kwamba eneo la historia ya shughuli
za dini na maingliano yake na serikali yakifanyiwa tafiti vizuri, yanaweza kuwa
chanzo kikubwa cha mapato ya serikali na sisi tunaona ukweli huo kwa kuanzia na
jambo hili.
2. Kwa
kuwa serikali sasa ina nguvu ya kujenga majengo ya shule nasi tumewapa mlango
wa kuchukua kodi hapa Mkunazini, tunaiomba sasa serikali iturudishie Shule ya
Mtakatiffu Monika ili kile ambacho kanisa inakipata baada ya kuondoa kodi,
turudishie kwa wazanzibar kwa kuandaa vizuri watoto wao.
3. Kwa
kuwa ziko kelele nyingi kuhusu ajira kwa vijana wa Kikristo kutopewa nafsi,
tunaishuri serikali ilifanyie kazi jambo hili kuleta usawa na kupunguza kelele.
Nafikiri niishie hapa kwa
leo, Mungu ibariki serikali ya Zanzibar, Mungu ibariki serikali ya Muungano wa
Tanzania, Mungu ibariki Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mungu ibariki Afrika,
Mungu bariki kanisa Anglikana popote lilipo. Amin.