Pages

Wednesday, March 16, 2016

KARIMJEE JIVANJEE YASAIDIA MATIBABU YA WATOTO WENYE SARATANI.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kulia) akimkabidhi Dk. Rehema Laiti cheti cha shukrani kwa kumaliza shahada ya uzamili katika matibabu ya saratani ya watoto na kwa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto. Katikati ni Dk. Trish Scanlan, Mwanzilishi wa Asasi ya Tumaini la Maisha.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kulia) akimkabidhi Dk. Shakilu Jumanne cheti cha shukrani kwa kumaliza shahada ya uzamili katika matibabu ya saratani ya watoto kwa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto. Katikati ni Dk. Trish Scanlan, Mwanzilishi wa Asasi ya Tumaini la Maisha.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kulia) akimkabidhi Dk. Moses Karashani cheti cha shukrani kwa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto wenye saratani. Katikati ni Dk. Trish Scanlan, Mwanzilishi wa Asasi ya Tumaini la Maisha.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na madaktari Moses Karashani aliyepewa nafasi ya kusoma uzamili wa kutibu saratani kwa watoto (kushoto) na Dk. Rehema Laitu (wa pili kushoto) na Dk. Shakilu Jumanne ambao walipatiwa vyeti vya shukrani kutokana na ubobezi katika matibabu ya saratani ya watoto.
 (Picha: Mpiga Picha Wetu)

 TAASISI ya Karimjee Jivanjee imetoa nafasi za masomo kwa madaktari watatu wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya mpango wake kuwajengea uwezo madaktari wa Tanzania ili waweze kuwa wabobezi katika matibabu ya saratani kwa watoto. 

Madaktari hao wamepewa fursa za kusomea shahada mpya ya uzamili katika matibabu ya saratani kwa watoto wadogo inayotolewa na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili. Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, amesema jijini Dar es salam leo kwamba taasisi hiyo inataka kuweka mazingira endelevu katika ubora wa huduma za afya kwa kuwajengea uwezo madaktari kuweza kuwatibu watoto wadogo wenye ugonjwa wa saratani. 

“Ili kutimiza lengo hili ni lazima wapatikane madaktari wenye sifa nchi nzima,” alisema Karimjee wakati akiongea kwenye hafla ya kuwapongeza madaktari waliomaliza kozi hiyo mwaka 2015 na wanaoanza kozi ya 2016 chini ya udhamini wa Karimjee Jivanjee Foundation.

 “Mwaka 2014, Tanzania haikuwa hata na daktari mmoja wa mwenye sifa za kutibu saratani kwa watoto lakini baada ya Daktari Trish Scanlan pamoja na Taasisi ya Tumaini la Maisha kuanzisha kozi hiyo ya uzamili kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, taasisi ya Karimjee iliona kwamba ni muda muafaka kutoa mafunzo kwa madaktari wa Kitanzania katika eneo hili na ndio maana tuliamua kusaidia program hii.” 

 Mwaka 2014 tulitoa nafasi za masomo kwa madaktari wawili kusomea kozi hiyo mpya na pamoja na mafunzo ya miezi mitatu nchini Ireland ili kupata uzoefu wa kimataifa ambapo kozi nzima iligharimu shilingi milioni 70. Madaktari walionufaika na program hiyo ni Dokta Rehema Laiti na Dk. Shakilu Jumanne ambao wamemaliza masomo na mafunzo yao na sasa wameajiriwa na Hospitali ya Taif ya Muhimbili kwenye kitengo cha saratani kwa watoto.

 Katika hafla hiyo, taasisi za Karimjee na Tumaini la Maisha waliwapatia madaktari hao vyeti vya shukrani kwa kazi wanayofanya kuokoa maisha ya watoto. Madaktari hao pia walizawadiwa shilingi milioni 6.6 kila mmoja ili waweze kuhudhuria kongamano la kimataifa kuhusu watoto wenye kansa litakalofanyika Dublin nchini Ireland Oktoba mwaka huu 2016. Taasisi ya Karimjee Jivanjee pia ilimtangaza Dokta Moses Karashani kuwa daktari atakayenufaika na programu hii kwa mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates